Back to Learning Plan
Mwokozi: Masomo yenye Athari Kubwa Kutoka Surah Al-Mulk
Day 2: Ukamilifu wa Uumbaji Wake
Mada: Kufahamu ukamilifu na utukufu wa Allah katika ulimwengu
Aya za Qur’ani
Somo na Tafakari
Katika aya hizi, Mwenyezi Mungu anatuelekeza macho yetu angani, akituhimiza kutazama, si mara moja tu, bali tena na tena uumbaji Wake. Ni kana kwamba Qur’ani inasema: weka mashaka yako, kiburi chako, madai yako ya uhuru kwenye mizani na uyalinganishe na Uumbaji kamilifu wa Allah. Chunguza mbingu kwa jicho la kukosoa zaidi uwezalo. Tafuta nyufa katika mpangilio, dosari katika ulinganifu, au kosa lolote lile katika usawa wa uumbaji wake.
Lakini hutapata hata moja. Yeye aliyeumba kila nyota angani, makundi ya nyota katika ulimwengu, kila upepo unaovuma, na kila tone la mvua linaponyesha, ameyaumba yote hayo — na zaidi ya hayo — kwa usahihi unaozidi uwezo wa kufikiri wa binadamu, zaidi ya ufahamu wa mwanadamu. Kuanzia mzunguko wa sayari hadi muundo wa mishipa ya jani, kila sehemu ya uumbaji inaelekeza moja kwa moja kwenye ukamilifu wa Muumba wake.
Hata kama mbunifu stadi zaidi anabuni kwa usahihi, uumbaji wa Mwenyezi Mungu unapita zaidi kwa kiwango kisichofahamika kwa binadamu: huo ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Macho yetu huchoka kabla ya kuona upungufu wowote, si kwa sababu umefichwa, bali kwa sababu haupo! Wanazuonii wanaelezea kwamba maneno mawili yaliyotajwa katika ayah: khāsiʾan na ḥasīr yanaelezea jinsi macho yanavyorudi yakiwa yamenyenyekea (kana kwamba yameshindwa au yametawanyika) na yamechoka kutokana na uchunguzi wa mara kwa mara, lakini haupati upungufu wowote.
Kama hii ndiyo hali ya maono unapojaribu kuelewa hata sehemu ya kile kilichoumbwa, basi binadamu anawezaje kutumaini kuelewa uhalisia kamili wa Muumba? katika utukufu Wake na uzuri Wake?! Subhanallah!
Ukamilifu huu hauko tu katika makundi ya nyota za mbali. Ni katika mapigo ya moyo wako, uwezo wako wa kupumua bila kufikiria, jinsi ngozi yako inavyopona kutokana na jeraha, na mwelekeo halisi wa dunia unaoruhusu uhai kustawi. Kila undani ni ishara, ikinong'ona: Hii haikuwa ajali. Hii ni kazi ya Al-Khaliq (Muumba), Al-Latif (Latifu kuliko wote), Al-Hakeem (Mwenye Hekima Yote).
Aya hizi zinatualika tuwe ni wenye kunyenyekea. Ikiwa uumbaji hauna dosari, basi hekima ya Muumba wake pia haina dosari, hasa katika matukio ambayo hatuelewi maishani mwetu. Mungu yule yule anayeweka nyota mahali pake anaweza kuweka maisha yetu katika usawa, hata wakati dhoruba za maisha zinapoonekana.
Kiini cha jambo: Kuuangalia uumbaji wa Allah kwa macho ya uhakika na yakini hugeuza ulimwengu kuwa ukumbusho wa nguvu na ukamilifu wa Mwenyezi Mungu wakati wote. Na unapoamini kuumba kwake kwa ulimwengu, basi itakua rahisi sana kwako kuamini muundo wake katika maisha yako. Aliumba ulimwengu mzuri sana, wenye usawa kiasi kwamba jicho lako huchoka kutafuta makosa. Lakini hauchoki kuvutiwa na uzuri wake.
Hadith ya Mtume (Rehema na amani zimshukie)
Mtume (Rehema na amani zimshukie) amesema:
“Allah alipanga vipimo vya uumbaji miaka elfu hamsini kabla ya kuumba mbingu na ardhi, na Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”
(Sahih Muslim 2653)
Hii inaonyesha kuwa kila undani wa uumbaji ulipangwa kwa hekima isiyo na mipaka kabla chochote hakijaumbwa.
Usisome tu, bali tenda…
Toka nje leo kwa dakika chache, kisha utazame anga. Iwe ni rangi ya bluu, imefunikwa na mawingu, au imejaa nyota. Tumia fursa hii kutafakari ukamilifu wa Allah. Jiambie:
“Mola anayeshikilia anga hii pana kwa ukamilifu, ndiye anayeshikilia maisha yangu pia.”
Faida zake:
- Inaufundisha moyo kutambua ishara za Allah kila siku (tafakkur).
- Inakuongezea tawakkul (kumtegemea Allah kikamilifu).
- Inaleta utulivu kupitia dhikr (kumkumbuka Allah).
Dua
رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَـٰطِلًۭا سُبْحَـٰنَكَ فَقِنَا عَذَابَ ٱلنَّارِ
Rabbanā mā khalaqta hādhā bāṭilan subḥānaka faqinā ‘adhāba an-nār.
“Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.”
(Qur’ani 3:191)
Tafakari hili:
Unapoona ukamilifu wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu, je, ni wasiwasi gani au mashaka uliyonayo yanapoteza uzito mbele ya nguvu na hekima Yake?