Back to Learning Plan
Uraibu wa Skrini: Skrini Zinapouiba Moyo
Day 3: Kulinda Macho, Masikio, na Moyo
Aya za Qur’ani
Somo na Tafakari
Kile tunachokiruhusu kupitia milango ya hisia zetu—tunachokiona, tunachosikia, na tunachokiweka nyoyoni—hakipiti bila athari; hutujenga. Skrini zimekuwa milango ya kila kitu: elimu yenye manufaa, lakini pia majaribu, kujilinganisha na wengine, wivu, kupoteza muda, na dhambi. Hisia zetu ni neema tulizopewa, na zinapaswa kuelekezwa kutumikia kusudi letu kuu: kumuabudu Mwenyezi Mungu.
Katika Surah Al-Isra (17:36), Mwenyezi Mungu anatukumbusha kwamba tutaulizwa kuhusu hisia zetu—kile tulichochagua kutazama, kusikia, na kukipa mioyo yetu. Na katika Surah Al-Munafiqun (63:9), Anatuonya tusiruhusu chochote, hata neema, kitutenge na kumkumbuka. Leo, kikwazo cha kawaida zaidi ni cha kidijitali: skrini zinazobadilisha mawasiliano ya kweli, kufifisha roho, na kuchelewesha yaliyo muhimu. Skrini zinaweza kuwa baraka zinapotumiwa kwa tija na kiasi; lakini matumizi kupita kiasi yanaweza kudhoofisha afya na ustawi wetu, na kutuacha tukiwa tupu kiroho. Nabii (rehema na amani zimshukie) alitushauri: “Jitahidi kutafuta yale yatakayokunufaisha.” (Sunan Ibn Mājah 4168)
Mwenyezi Mungu anatukumbusha kwamba macho, masikio, na moyo ni amana tutakazoulizwa kuhusu matumizi yake. Je, tunawajibika kila mara 'tunaposcroll' (kutazama na kupitia skrini bila kikomo)? Tunaruhusu nini kuingia? Tunazilisha nini nyoyo zetu? Tunazipa roho zetu nini? Historia imetuonyesha kwamba kuendelea kushikilia wazo fulani, hata liwe ovu kiasi gani, huleta kulikubali na kulihalalisha kadri muda unavyopita. Fitrah(umbile la ndani lililokuwa safi na lenye mwelekeo wa kumtambua na kumuabudu Mwenyezi Mungu) linaweza kuharibika kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya mawazo potofu. Kutazama na kupitia skrini bila kikomo ni mojawapo ya fitina inayokubalika zaidi leo—na huenda ndio inayoharibu zaidi.
Katika Surah An-Nur (24:30), Mwenyezi Mungu anawaamuru Waumini wanaume (na wanawake katika aya inayofuata) wainamishe macho yao—si tu dhidi ya uchi, bali dhidi ya chochote kinachochafua roho. Sio kila chapisho linalovuma, maelezo, au taswira linahitaji macho yetu. Kulinda macho si kuepuka dhambi tu; ni kulinda moyo—chombo kinachobeba mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Na mapenzi haya hayawezi kuishi pamoja na mapenzi ya matamanio ya upuuzi.
Kila jambo tunaloruhusu kupitia hisia zetu ima hupooza au hukaza moyo. Ihsan katika matumizi ya skrini ni kuchagua kwa mazingatio: kuangalia kwa kusudi, kusikiliza kwa umakinifu, na kuhifadhi usafi wa moyo. Usiruhusu skrini iufanye moyo wako kuwa na ganzi. Tumia neema zako kwa hekima—kuanzia hisia zako hadi skrini zako. Jiulize: je, hili limenikaribisha kwa Muumba wangu, linanihimiza kuswali, na kutimiza wajibu wangu kama Muislamu, au limenitenganisha na hayo?
Hadithi ya Mtume (rehema na amani zimshukie)
Nabii Muhammad (rehema na amani zimshukie) alisema:
“Anapomwangalia mmoja wenu mtu aliyemzidi kwa mali au kwa sura, basi na amwangalie pia aliye chini yake.”
(Sahih al-Bukhari, Hadithi 6490; Sahih Muslim, Hadithi 2963)
Hekima hii ina nguvu kubwa katika mitandao ya kijamii na kujilinganisha mtandaoni. Ni ukumbusho wa kudumu kwamba wapo wengi wasio na hata fursa hizi. Tunapaswa kushukuru kwa neema zetu na kutozitumia vibaya.
Usisome tu, bali tenda…
Chuja Machapisho Yako: Pitia maudhui ya skrini zako, hasa mitandao ya kijamii. Ondoa ufuatiliaji au nyamazisha chochote kinachokuonesha mara kwa mara uchi, wivu, au usumbufu. Tengeneza nafasi ya nuru, si kelele.
Dua
“Ewe Mwenyezi Mungu, linda macho yangu na yale yanayokukasirisha, masikio yangu na kelele zenye madhara, na moyo wangu na chochote kinachonitenga na Wewe.”
Tafakari hili
Ni nini ninachokaribisha kila siku kupitia skrini zangu kuingia machoni, masikioni, na moyoni—na je, kinanisongeza karibu au kunitenganisha na yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka niwe?